Jumapili, 26 Juni 2016

Lessoni jumapili

*JUMAPILI  JUNE 36 2016*

*MFANO WA MUNGU*

Biblia inasema kuwa, kwa asili, mwanadamu aliumbwa kwa mfano wa Mungu. (Mwanzo 1:27). Umbo linaweza kuwa la kutazamwa kwa pande mbili, kama vile kuakisi kwa kioo au nakala ya picha, au kutazamwa kwa pande tatu, kama vile sanamu au picha ya pande tatu inaytokana na maingiliano ya mionzi ya nuru. Wakati mwingine sura au mfano huwa ni kitu kisicho halisi, kama vile picha ya mawazoni, dhana tunayokuwa nayo akilini. Biblia inamaanisha nini?

*Soma Mwanzo 1:26, 27. Maandiko yanafafanuaje juu ya kuumbwa kwa sura ya Mungu? Angalia pia Mwanzo 1:31, Kumb. 6:5, na 1Thes. 5:23.*

Kwa kuumbwa kwa wazazi wetu wa kwanza, Mungu aliweka kiwango kipya kwa ajili ya maisha duniani: mwanamume na mwanamke. Wao peke yao, miongoni mwa viumbe vingine vyote vilivyoumbwa wakati huo, walikuwa na mfano wa Mungu. Hawakuwa manyani waliobadilika na kuwa binadamu. Kama Wanadamu, wao pamoja na sisi kimsingi tuko tofauti kabisa na aina zingine zote za viumbe duniani, na teolojia yoyote inayohafifisha tofauti hii inamdhalilisha mwanadamu.

"Mungu akawaita jina lao Adamu" (Mwanzo 5:2). Yaani, wote wawili mwanamume na mwanamke, ijapo wako tofauti kabisa kila mmoja kwa mwenzake, hata hivyo bado walikuwa ni mmoja. Kwa pamoja, katika ukamilifu na utimilifu wao, walikuwa wakiiwakilisha sura ya Mungu.

Asili ya sura ya Mungu ni jumuishi: "Adamu alipotoka katika mikono ya Mwumbaji, alikuwa amebeba, katika asili yake ya kimwili, kiakili, na kiroho, mfano wa Muumba wake." - Ellen G. White, Education uk. 15.

Neno linalosimama "sura" katika Kiebrania ni tselem; na neno linalosimamia "mfano" ni demuth. Maneno hayo yanaweza kumaanisha umbile la kimwili na kiakili vya mwanadamu. Ellen G. White analitambua hilo anaposema mwanadamu aliumbwa katika sura ya Mungu "ni katika kufanana kwa sura ya nje na katika tabia pia." - Patriachs and Prophets, uk. 45.

Kumbukumbu la Torati 6:5 huzitaja nyanja mbalimbali zilizomo ndani ya mwanadamu: roho (mambo ya kiroho), moyo (akili, utambuzi), na nguvu; (yaani mwili). Kuna mpangilio kama huo pia katika 1Thes. 5:23. Mwanadamu aliyeumbwa kwa sura ya Mungu kwa asili angejumuisha vitu vyote hivyo vyote ndani yake.

*"Ijapokuwa Kuna mengi zaidi juu ya dhana hii ya kuumbwa katika "sura ya Mungu," Biblia iko wazi kuwa: binadamu ni kiumbe tofauti na wa pekee katika viumbe vyote hapa duniani. Hakuna kiumbe kingine chochote kilicho karibu naye. Kwa nini ni muhimu kwetu kuidumisha tofauti hiyo akilini?*

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni