Jumapili, 5 Juni 2016

Matukio ya Siku za Mwisho.

(Mathayo 23 & 24)

Utangulizi:
Mojawapo ya faida maridhawa
ya kuandika masomo haya ni kwamba
yananilazimisha kujifunza Biblia. Malengo
makuu ya kuandika masomo haya ni
kuiboresha Shule ya Sabato na kuwasaidia
wanafunzi kuyaelewa mapenzi ya Mungu
vizuri zaidi. Hata hivyo, ninapojifunza Biblia
mara zote huwa ninafikiria juu ya athari za
neno la Mungu maishani mwangu. Juma hili
baadhi ya kauli za Mathayo zinaingiliana
sana na maisha yangu binafsi kiasi kwamba
natangulia kuomba radhi kwa kujihusisha
sana katika somo hili. Hebu tuchimbue zaidi
na tuone kama wewe pia unajisikia
kujihusisha na somo letu la Biblia!

I. Walafi wa Sifa
A. Soma Mathayo 23:1-4.
Unapotambua kwamba mtu fulani ni
mnafiki, je, unayachukuliaje mafundisho ya
mtu huyo? (Wazo la jumla ni kuyakataa
mafundisho ya mtu mnafiki.)

1. Kwa nini Yesu anasema kuwa
wanafiki hawa waheshimiwe? (Kwa sababu
“wanaketi katika kiti cha Musa.”)
a. Hiyo inamaanisha nini, na
kwa nini jambo hilo ni muhimu sana?
(Nadhani inamaanisha kwamba
wanafundisha torati iliyotolewa na Mungu
kupitia kwa Musa.)

2. Nawakumbuka viongozi wa
dini kadhaa maarufu waliokuwa na dhambi
maarufu. Mwitiko wangu ulikuwa ni
kwamba waliikumbatia na kuikubali dhambi
– jambo ambalo ni kweli kwetu sote.
Tunawezaje kuwatofautisha wale viongozi
wa dini “walioketi katika kiti cha Musa” na
wale wanaotupotosha? (Sababu kuu ya
kuanza na maswali yanayotokana na fungu
la Biblia katika mfululizo wa masomo haya
ni kwamba hatuwezi (natumaini hivyo)
kupotoka sana ikiwa tutajikita kwenye neno
la Mungu. Suala la muhimu zaidi ni endapo
kiongozi anafundisha Biblia au anafundisha
kitu kingine kabisa.)

B. Soma Mathayo 23:5-7. Kuwa
mwaminifu. Je, unapenda kutukuzwa,
pamoja na kupewa kiti bora kabisa? Je,
unapenda kusalimiwa na watu
wanaokuheshimu? (Ikiwa umesema
“hapana,” nadhani tu kwamba umevunja
Amri ya Tisa. Sote tunapenda kutukuzwa/
kuheshimiwa.)
1. Tunawezaje kuepuka kuwa
kama hawa viongozi wa dini? (Angalia tena
fungu la 5, “matendo yao yote huyatenda ili
kutazamwa na watu.” Ikiwa kila jambo
unalolitenda linahamasishwa na kujitukuza
kwako, tofauti na kumpa Mungu utukufu au
kumpenda mtu mwingine, basi una tatizo
kubwa.)

C. Soma Mathayo 6:2. Nini
maana ya “wamekwisha kupata thawabu
yao?” Je, inamaanisha kwamba “thawabu
kamili” ni kujitukuza binafsi –
itakayokukosesha mbingu? (Napenda
kuhubiri, ninapenda kufundisha, na hakuna
shaka yoyote kwamba sehemu ya sababu
yangu ni kwamba ninataka watu wamjue
Mungu vizuri zaidi. Lakini, sehemu nyingine
ya sababu zangu ni kwamba ninapenda
watu waseme kuwa, “anafanya kazi nzuri.”
Ninaposoma habari za hawa viongozi wa
dini ambao thawabu yao pekee ipo hapa,
ninasikitika. Dkt. William H. Shea ni
mmojawapo wa Wakristo wa pekee kabisa
niliowahi kuwafahamu. Ni mwerevu sana
na mnyenyekevu kupindukia. Nilimuuliza,
“Je, unafurahia heshima/sifa unayopewa
kwa kuhubiri na kufundisha?” Alijibu,
“ndiyo,” hiyo ni sehemu mojawapo. Hiyo
iliufanya moyo wangu utulie katika suala
hili.)

D. Soma Mathayo 23:8-12.
Mmojawapo wa wanafunzi wangu wa
zamani alikuwa akiniita “rabi” na mara kwa
mara mke wangu huniita “profesa.”
Wanangu wananiita “Baba.” Wanafunzi
katika shule ya sheria huniita “Profesa
Cameron.” Je, ninapaswa kuwaambia wote
hawa waache kuniita hivyo?

1. Soma Kutoka 20:12. Suala
mojawapo ni kuwaheshimu viongozi wa
dini. Fungu hili linatuambia tuwaheshimu
wazazi wetu – na hiyo inajumuisha kumuita
baba yangu kuwa “Baba.” Unawezaje
kuelewa mkanganyiko wa dhahiri uliopo
kwenye Biblia?

2. Kumbuka muktadha. Je,
viongozi wa dini wananyakua heshima gani
isivyostahili? (Wanadai heshima
inayomstahili Mungu. Wanafanya kila jambo
kwa ajili ya utukufu wao, na sio utukufu wa
Mungu au upendo kwa watu wengine.
Utagundua kwamba katika Mathayo 23:8-10
anayepaswa kurelejewa ni Mungu.
Wanangu, mke wangu, wanafunzi wangu
hawadhani kwamba mimi ni Mungu na
sijaribu kuwachanganya akili katika jambo
hilo.)

E. Hebu turuke mafungu kadhaa
hadi Mathayo 23:37-39. Tatizo la msingi la
viongozi wa dini Yerusalemu lilikuwa ni
lipi? (Walimkataa Yesu. Utaona kwamba
mjadala wa “mada” ni sehemu ya kumkataa
Yesu. Sasa Yesu anasema kuwa mwisho wao
umefika. Hawako radhi kumkubali au
kumpa utukufu.)

II. Kubomolewa

A. Soma Mathayo 24:1. Unadhani
kwa nini wanafunzi walimwambia Yesu
aangalie majengo ya hekalu? (Pasi na shaka
majengo hayo yalikuwa mazuri. Nimesoma
maelezo ya Josephus kuhusu hekalu na
maelezo hayo yalikuwa mazuri ajabu.)

B. Soma Mathayo 24:2-3. Bila
shaka habari hii ni ya kutisha. Kwa nini
wanafunzi walimwendea Yesu kwa
“faragha” ili kutaka kufahamu habari kwa
kina zaidi?

1. Unaona maswali mangapi
katika mafungu haya? Unadhani wanafunzi
walidhani walikuwa wanamuuliza Yesu
maswali mangapi? (Nadhani walikuwa
wanauliza angalao maswali mawili, lakini
nadhani walidhani kwamba walikuwa
wanauliza swali moja tu. Bila shaka
walidhani kuwa hekalu halitabomoshwa
hadi Yesu atakaporejea “mwisho wa
dahari.”)

III. Mwisho

A. Soma Mathayo 24:4. Yesu
anajali jambo gani kwanza? (Kwamba
tuepuke kudanganywa/kulaghaiwa.)

B. Soma Mathayo 24:5-14. Mara
tatu Yesu anarejea “nyakati za mwisho”
katika hivi vifungu. Anajadili mwisho gani,
mwisho wa hekalu au mwisho wa dunia?

C. Soma Mathayo 24:15-20.
Unadhani jambo gani linajadiliwa hapa? (Ni
kawaida kwamba unabii unaweza
kutimizwa zaidi ya mara moja. Lakini hii
inaonekana kuendana na kubomolewa kwa
Israeli. Wakristo wengi waliukimbia mji na
waliokolewa kabla ya hekalu kuangamizwa
na Warumi.)

D. Soma Mathayo 24:23-27. Jambo
gani linaelezewa hapa? (Ujio wa Yesu Mara
ya Pili.)

1. Kuna jambo gani mahsusi
kuhusu Wakristo kudanganywa? (Watatokea
makristo wa uongo – na ishara zao na
miujiza yao ina ushawishi mkubwa sana.)

2. Tunawezaje kuepuka
kudanganywa? (Hakuna mtu atakayetakiwa
kutuambia kuhusu ujio wa Yesu Mara ya
Pili. Watu wote watauona kwa mara moja.
Nimeepuka baadhi ya masuala magumu
zaidi kwenye ujumbe wa Yesu kwa sababu
ninaweza kukosea. Hata hivyo, sehemu
rahisi ya ujumbe huo iko dhahiri kabisa –
utafahamu tu Yesu atakapokuja!)
a. Kwa nini basi Yesu anatuonya
kwamba tunatakiwa kuepuka kudanganywa,
na kwamba uongo ujao utakuwa na nguvu
kubwa sana? (Tuna nafasi kubwa sana ya
kudanganywa na hao walaghai. Ikiwa
unajihusisha kwenye mjadala unaomhusisha
mtu fulani kwamba ni Yesu, basi huo ni
uthibitisho madhubuti kwamba mtu ni
mlaghai na si Yesu!)

E. Soma Mathayo 24:30-31 na
Mathayo 24:40-41. Je, tutakuwa na
uthibitisho gani mwingine kamili kuhusu
ujio wa Yesu Mara ya Pili? (Watakaookolewa
watachukuliwa mbinguni!)

1. Je, “sauti ya parapanda”
inahusu nini? (Soma 1 Wakorintho 15:51-52.
Wale waliokufa wakimtumaini Yesu
watafufuliwa kwa dakika moja, kufumba na
kufumbua wakati wa mlio wa parapanda.)

F. Hebu tupitie mambo yote
haya ili usiweze kudanganywa. Jambo gani
litatokea Yesu atakapokuja tena? (Mwanga
kama wa radi utatokea duniani kote – kila
mtu atauona kwa wakati mmoja. Waliokufa
katika Kristo watafufuliwa kutoka
makaburini. Watakaookolewa wakiwa hai
watakuchukuliwa mbinguni.
Hautachanganyikiwa kuhusiana na hili
tukio. Ikiwa hutachukuliwa mbinguni, hiyo
ni habari mbaya sana.)

G. Soma Mathayo 24:42-44. Hebu
subiri kidogo, hivi punde tu tumejifunza
kwamba ujio wa Yesu Mara ya Pili utakuwa
dhahiri kwa kila mtu. Kwa nini tunaonywa
“kukesha” na kuhusu matatizo ya ujio wa
ghafula? Ninaweza kuwa kwenye usingizi
mzito lakini sitaweza kuukosa ujio wa Yesu
Mara ya Pili! (Mwizi havunji na kuingia
nyumbani kwa Yesu katika huu mfano.
Mwizi anavunja na kuingia nyumbani
kwako. Onyo halihusu utata juu ya ujio wa
Yesu, bali endapo u tayari!)

H. Soma Mathayo 24:45-46.
Unapaswa kuwa unafanya nini wakati
ukiutarajia ujio wa Yesu Mara ya Pili? (Kazi
yako – “kuwalisha” watumishi wa Yesu.
Tunatakiwa kuendelea kufanya kazi ili
kuuendeleza Ufalme wa Mungu!)

I. Rafiki, viongozi wa dini
walikuwa na tatizo gani tulilolijadili
mwanzoni mwa somo hili? Tatizo ni
kwamba walikuwa wanafanya kazi ya
kuuendeleza utukufu wao wenyewe. Yesu
anatupatia wito wa kufanya nini wakati
tunasubiria kurudi kwake? Kuuendeleza
Ufalme wa Mungu. Je, unafanya nini siku
hizi? Je, unauendeleza utukufu wako au
Ufalme wa Mungu? Ikiwa hulipendi jibu
lako, kwa nini usitubu sasa hivi na
umwombe Roho Mtakatifu akuoneshe njia
bora zaidi?

IV. Juma lijalo: Siku za Mwisho za
Yesu.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni