Ni mwendelezo wa somo la kupajenga
palipobomoka, usisite kutoa maoni yako kupitia sehemu ya maoni hapo
chini kwa masiliano zaidi piga simu 0712672894
5. MPANGO WA MUNGU KATIKA MAKUSANYIKO YA KIROHO.
Limeandaliwa na Basilio Maliwanga mhazini TUCASA-STUM
Limeandaliwa na Basilio Maliwanga mhazini TUCASA-STUM
“wala tusiache kukusanyika pamoja, kama ilivyo desturi ya wengine; bali tuonyane; na kuzidi kufanya hivyo, kwa kadiri mwonavyo siku ile kuwa inakaribia.” Waebrania 10:25
UTANGULIZI NA MAANA YA KUSANYIKO LA KIROHO.
Mtunzi wa zaburi huanza katika sura ya 133 kwa kuema, “Tazama, jinsi ilivyo vema, na kupendeza, Ndugu wakae pamoja, kwa umoja.”fungu la 1. Mungu hufarahia pale ambapo watu wake hukutana na kukaa kwa pamoja kwa ajili yake. Ni haja ya Mungu kwamba mara kwa mara watu wake wakusanyike ili kuwa karibu nao.
Kusanyiko ( kwa kiingereza “assembly” au “congregation”) katika biblia hutokana na neno la kiebrania “qahal” au “ edah” (ambalo lilikuwa na maana ya kusanyiko takatifu la wanaisraeli lililowekwa kwa ajili ya shughuli takatifu ya kidini), na neno la kigiriki “sunago”( ambapo tunapata neno sinagogi).
Neno hili humaaanisha, mjumuiko wa watu katika eneo moja, waliokutana kwa lengo au kusudi moja. Webster anaelezea kusanyiko kama, kukutanika kwa kundi la watu kwa lengo la kumwabudu Mungu au kwa kufuata maelekezo ya kidini.1
MAKUSANYIKO KATIKA BIBLIA.
Biblia huonyesha kuwepo kwa makusanyiko katika zama zote yaani agano la kale na agano jipya. Katika agano la kale tunawaona wana Israeli wakikusanyika kwa pamoja kama ilivyo agizo la Mungu na kwa makusudi maalumu ya MUNGU. Katika Kutoka 12 tunaona Mungu akiwaagiza Israeli kukusanyika kwa pamoja siku ya kwanza na siku ya saba wakati akiandaa mpango wa ukombozi wao kutoka Misri. Hata walipokuwa jangwani katika kipindi cha miaka 40 Mungu aliwaagiza Israeli pia kukusanyika mara kwa mara mbele ya hema ya kukutania kwa makusudi mbalimbali ya kidini. Katika sikukuu mbalimbali za wanaisraeli kulihusisha watu kukusanyika kwa pamoja mara kwa mara (ambapo biblia huyaita makusanyiko matakatifu, walawi 23:4) kwa makusudi maalumu. (Soma Mambo ya walawi 23). Hata kipindi cha mitume
1 Noah Webster‟s Dictionary of 1828.
KUPAJENGA PALIPOBOMOKA NA KUPASIMAMISHA UPYA 2014/2015
TUCASA | Southern Tanzania Union Mission 15
pia kulikuwa na makusanyiko mbalimbali ya kiroho ambapo watu walikuwa wakikutana katika masinagogi au majumbani kwa lengo au kusudi maalumu la kiroho (Matendo 12:12)
KWANINI MUNGU HUTAKA WATU WAKE WAKUSANYIKE KWA PAMOJA?
1. Kwa ajili ya kukutana nao katika makusanyiko hayo. Makusanyiko ni njia mojawapo ambayo MUNGUameiweka ili akutane na watu wake na kuwajenga kiroho.
2. Kumjifunza MUNGU kwa njia ya kujifunza neno lake. Katika mathayo 5 (wengi hupenda kuiita hotuba ya mlimani), Yesu alikuwa mlimani pamoja na kusanyiko kubwa sana la watu ambao wamekaa wakiwa wanamsikiliza kile ambacho anakisema. Biblia huanza kwa kusema, “Naye alipowaona makutano, alipanda mlimani; na alipokwisha kuketi wanafunzi wake walimjia; akafumbua kinywa chake, akawafudisha” fungu la 1 na 2. Mwalimu huyu mkuu alikuwa akitumia makusanyiko haya kwa lengo la kuwafundisha watu neno la MUNGU pamoja na kuwatoa katika vifungo vyao kwa njia ya neno hilo. Lakini hata mitume walitumia makusanyiko kwa ajili ya kufundishana neno la MUNGU wao kwa wao, lakini pia kwa wasioamini. Katika matendo sura ya 10 tunamuona Petro katikati ya kusanyiko katika nyumba ya kornelio,” Na Kornelio alikuwa akiwangojea, hali amekusanya jamaa zake na rafiki zake”fungu la 24. Petro alifundisha neno la MUNGU nyumbani kwa kornelio na mwisho watu hawa walibatizwa. (soma pia Matendo 17:1-4)
3. Mungu kudhihirisha nguvu na uweza wake kwa wanadamu ili wapate kuamini na kupata wokovu. Katika matendo 2 baada ya wanafunzi wa Yesu kukaa orofani na kusali na kuomba, katika siku ya pentekoste Mungu alidhihirisha nguvu zake na uwezo wake katika kusanyiko lao baada ya kumwaga nguvu ya Roho mtakatifu juu yao. Biblia huanza kwa kusema, “Hata ilipotimia siku ya pentekoste walikuwako wote mahali pamoja.”fungu la 1. Lakini kwa upande mwingine, Mungu pia alidhihirisha nguvu na uwezo wake hata katika watu ambao walikuwa hawaamini na hawana habari yoyote juu ya Yesu waliokuwepo Yerusalemu. Baada ya mitume kujazwa nguvu ya Roho mtakatifu “wakaanza kusema kwa lugha nyingine kama Roho alivyowajalia kutamka”. Lugha walizokuwa wanazizungumza zilikuwa za watu wa mataifa mbalimbali waliokuwepo mahali pale. Kusanyiko lile lote likashikwa na mshangao. Lakini petro akasimama na kuanza kuihubiri Injili ya Yesu kwa watu hawa. Paulo anaandika anasema, “Kwa maana
KUPAJENGA PALIPOBOMOKA NA KUPASIMAMISHA UPYA 2014/2015
TUCASA | Southern Tanzania Union Mission 16
siionei haya Injili; kwa sababu ni uweza wa Mungu uuletao wokovu, kwa kila aaminiye, kwa Myahudi kwanza, na kwa Myunani pia.” Rumi 1:16. Neno “uweza” lililotumika hapa ni neno la kiyunani “Dunamis” ambalo humaanisha nguvu iwezayo kutenda miujiza na maajabu, nguvu yenye uwezo mkubwa wa kubadilisha kitu au mtu. Ndio maana tunaona baada ya Petro kumaliza mahubiri yake katika kusanyiko hili watu 3,000 walibadilishwa na kufanywa upya nia zao na kumwelekea Kristo.
4. Kumwekea Mungu haja zetu na kufanya maombi. Katika makusanyiko pia kunaweza kuwa ni mahali ambapo watu wa MUNGU huweza kufanya maombi na kumwekea MUNGU haja zao. Katika matendo 1 tunaona Yesu akiwapa agizo wanafunzi wake kabla ya kupaa, juu ya kukusanyika pamoja Yerusalemu na kutokutoka nje ya Yerusalemu. Biblia huonyesha kuwa wanafunzi walikusanyika kwa pamoja orofani “wakidumu kwa moyo mmoja katika kusali” fungu la 14. Katika kusanyiko hili sio tu kwamba wanafunzi walikusanyika bali walikuwa wakisali na kumwomba Mungu. Vilevile tunamuona Mfalme Yehoyakimu akiwakusanya wanaisraeli na Yuda kwa ajili ya kumwomba na kumsihi MUNGU awaokoe juu ya majeshi ya wana wa Moabu na Amoni waliojipanga kupigana na Israeli. Biblia inasema, “Yuda wakakusanyika kwa pamoja ili wamtafute BWANA, hata kutoka miji yote ya yuda wakaja kumtafuta BWANA.” 2nyakati 20:4 (soma 2nyakati 20:1-13). Yesu aliwaambia wanafunzi wake kuwa, “Tena nawaambia, ya kwamba wawili wenu watakapopatana duniani katika jambo lo lote watakaloliomba, watafanyiwa na Baba yangu aliye mbinguni, Kwa kuwa walipo wawili watatu wamekusanyika kwa jina langu, nami nipo papo hapo katikati yao.” Mathayo 18:19, 20. Kwa maana nyingine Yesu anasema mnaweza kukusanyika wawili watatu na kufanya maombi na Baba yangu wa mbinguni atawasikia na kuwajibu.
5. Kutoa shukrani kwa Mungu: Mungu hutumia makusanyiko ya kiroho kama njia mojawapo ambapo watu wake huweza kutoa shukrani zao kwa kile ambacho wametendewa na MUNGU, Kumbukumbu la torati 16:16, “Mara tatu kwa mwaka na watokee wanawaume wako wote mbele za Bwana, Mungu wako, mahali atakapochagua; katika sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu, na katika sikukuu ya majuma, na katika sikukuu ya vibanda; wala wasitokee mbele za Bwana mikono mitupu.” Hapa tunaona Mungu akiwaagiza Israeli ili kukutanika mara tatu kwa mwaka lakini akiwaambia “wala wasitokee mbele za Bwana mikono mitupu.” Maana yake waje na matoleo mbalimbali
KUPAJENGA PALIPOBOMOKA NA KUPASIMAMISHA UPYA 2014/2015
TUCASA | Southern Tanzania Union Mission 17
kwa ajili ya kutoa shukrani zao kwa BWANA. Kusanyiko takatifu la sikukuu ya vibanda lilikuwa maalumu kwa wana Israeli kuja kumtolea Mungu wao dhabihu kama shukrani kwa kile alichowatendea kwa kipindi cha mwaka mzima. “From far and near the people came, bringing in their hands a token of rejoicing. Old and young, rich and poor, all brought some gift as a tribute of thanksgiving to Him who had crowned the year with His goodness, and made His paths drop fatness.” 2
MAMBO MUHIMU YA KUZINGATIA UNAPOPANGA KUHUDHURIA KATIKA MAKUSANYIKO.
1. Ni lazima uombe ili uwepo wa MUNGU uwepo katika kusanyiko hilo: Biblia husema, “Kwa kuwa walipo wawili watatu wamekusanyika kwa jina langu, nami nipo papo hapo katikati yao” Mathayo 18:20. Mahali pengine husema, “Basi “Bwana”; ndiye Roho; walakini alipo Roho wa Bwana, hapo ndipo penye uhuru. 2korintho 3:17. Ni lazima tuhakikishe kuwa katika kusanyiko hilo panafunikwa na kuzungukwa na uwezo na nguvu za Mungu. Kumbuka lengo mojawapo la makusanyiko ni ili watu wa Mungu wawekwe huru kutoka katika vifungo vyao mfano, vifungo vya maradhi, dhambi n.k. kwa hiyo ni muhimu sana kabla ya kuhudhuria katika kusanyiko lolote lile kumuomba Mungu awepo na kutangulia katika kusanyiko hilo. Daudi anaandika katika zaburi 16:8 anasema, “Nimemweka Bwana mbele yangu daima, Kwa kuwa yuko kuumeni kwangu, sitaondoshwa.”
2. Kujua hasa kusudi la Mungu kwako „binafsi‟ katika kuhudhuria katika kusanyiko hilo: Ijapokuwa tumeona kuwa kuna makusudi mbalimbali ya Mungu katika makusnyiko haya ya kiroho, lakini kwa upande mwingine Mungu huwa na makusudi tofauti tofauti kati ya mtu mmoja na mwingine katika kuhudhuria makusanyiko haya ya kiroho. Hivyo ni jambo la muhimu sana kumuuliza Mungu wewe binafsi kile alichokipanga juu yako katika kusanyiko hilo la kiroho. Ijapokuwa kuna makusudi ya ujumla (General purposes) lakini kumbuka kuwa kuna makusudi maalumu ya mtu mmoja mmoja (Special purposes) ya MUNGU katika makusanyiko haya.
2 White .E. G. ( ). Tumaini la vizazi vyote.
KUPAJENGA PALIPOBOMOKA NA KUPASIMAMISHA UPYA 2014/2015
TUCASA | Southern Tanzania Union Mission 18
HITIMISHO.
Biblia inasema, “Pasipo maono, watu huacha kujizuia; Bali ana heri mtu yule aishikaye sheria.” Mithali 29:18 maana yake tusipojua kwa hakika ni nini ambacho Mungu amepanga tukutane nacho katika kusanyiko hilo tutashindwa kujizuia (kiingereza fungu hili huandikwa, Where there is no vision, the people perish [KJV]). Shetani anaweza kutumia mwanya huo wakutokufahamu hasa kusudi la MUNGU kwangu na kwako ili kutuangamiza.
Petro hutukumbusha kuwa, “Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze.” 1petro 5:8.Tukumbuke kuwa shetani yupo wakati wote akitutamani sana kutumaliza na kutupoteza, hivyo hata tunapokuwa katika makusanyiko mbalimbali ya kiroho hukaa karibu akimtafuta mmoja asiyejua hasa kwanini yupo katika kusanyiko hilo amrubuni na kumpatia malengo au makusudi yake yeye mwenyewe katika kusanyiko hilo.
Liwe ombi la kila mmoja wetu kwa MUNGU ili atufunilie ni kipi hasa anataka tukutane nacho katika makusanyiko mbalimbali ya kiroho.
Mungu atubariki na kutusaidia tunapojiandaa kuhudhuria katika makusanyiko mbalimbli ya kiroho na kukutana naye huko. Amen . INAENDELEA..................
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni